0
Chama cha walimu (CWT) wilaya ya Makete kimeitaka serikali kuwalipa madeni yao wanayoidai kwa kuwa yanapokaa muda mrefu inapelekea kuvunjika moyo wa kuendelea kufundisha kama inavyotakiwa

Sanjari na hayo wamewakumbusha walimu wote nchini kuhakikisha wanatimiza wajibu wao kwa kufundisha kwa juhudi na maarifa yao yote kama inavyotakiwa na serikali pamoja na kanunia na taratibu za kiutumishi zinavyoelekeza

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Makete mkoani Njombe Bw. Thobias Kasambala wakati wa hafla ya kuwakabidhi bati 20 kila mmoja walimu 6 waliostaafu kati ya Julai na Septemba mwaka huu iliyofanyika katika ukumbi wa kata ya Iwawa Makete mjini

"Tumechoka kusikia maneno matamu, tunataka vitendo, serikali imekuwa ikidaiwa na walimu, na hata hapa wilayani kwetu wapo wanaodai stahiki zao kutoka kwa serikali, tunaiomba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ione namna ya kutulipa madai yetu" amesema Kasambala

Kaimu Afisa elimu Msingi wilaya ya Makete Bw. Leopord Mlowe amesema kustaafu sio laana au mkosi bali ni jambo la heri ambalo watu wengi wamekuwa wakilitamani hivyo baada ya wao kustaafu wanatakiwa kuangalia na kujichagulia shughuli mbalimbali ambazo watakuwa wakijishughulisha nazo kipindi hiki ambacho wamestaafu

"Ninyi ni walimu wazuri tu na bahati nzuri walimu wa zamani mnasifika kuwa na maadili mazuri, mnaweza kuanzisha madarasa yenu huko mnakoenda na kuwafundisha watoto maana ujuzi mlionao hauzeeki na ualimu wenu mtaendelea kukaa nao mpaka siku Mungu atakapoamua kuwachukua" amesema

Awali katibu wa CWT Wilaya ya Makete Elizabeth Sikawa amesema mpango huo umeanza rasmi mwaka huu na kusema kuwa suala hilo ni baada ya mapendekezo ya muda mrefu yaliyotolewa na wanachama hao ingawa linatekelezwa mwaka huu

"Unajua si kila anayeanzisha jambo ni lazima yeye afaidi matunda yake, Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake alianzisha mambo mengi lakini hajayafaidi na matokeo yake kinafaidi kizazi hiki cha sasa, nitataja mambo mawili, alishiriki kuanzisha msitu ambao upo pale Mafinga Iringa, na Msitu mwingine uliopo Rongai wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, lakini tunaofaidi ni sisi na yeye alishafariki dunia" amesema Sikawa

Amesema wastaafu hao kila mmoja amepatiwa bati 20 ambapo ndio utaratibu mpya wa chama hicho kuwashika mkono wa kwaheri walimu wastaafu kila baada ya miaka mitatu

Baadhi ya walimu hao waliostaafu wamesema wanafurahia kitendo hicho cha kupatiwa zawadi baada ya kustaafu na kusema kitaamsha ari na moyo wa walimu kujituma kwa bidii zaidi kufundisha, pamoja na kujitunza ili wafikie hatua ya kustaafu kama wao

Post a Comment

(function(i,s,o,g,r,a,m){i['GoogleAnalyticsObject']=r;i[r]=i[r]||function(){ (i[r].q=i[r].q||[]).push(arguments)},i[r].l=1*new Date();a=s.createElement(o), m=s.getElementsByTagName(o)[0];a.async=1;a.src=g;m.parentNode.insertBefore(a,m) })(window,document,'script','https://www.google-analytics.com/analytics.js','ga'); ga('create', 'UA-87191200-1', 'auto'); ga('send', 'pageview'); ga('set', 'userId', {{USER_ID}}); // Set the user ID using signed-in user_id.
 
Top