0

Ni kutengeneza utajiri kirahisi, lakini kuhatarisha maisha ya watu.

Madaktari waliosomea sayansi ya tiba hungaika kufanya vipimo mbalimbali kuchunguza chanzo cha ugonjwa kabla ya kutoa tiba, lakini waganga wa tiba mbadala hawahangaiki; wanachunguza kwa dakika zisizozidi mbili, kupata majibu na kutoa tiba.

waganga hao, ambao sasa wanatamba kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni hasa nyakati za usiku, wanafanya uchunguzi huo kwa kutumia Kifaa kinachoitwa Quatum Magnetic Analyser, ambacho watengenezaji wake wanadai hufanya uchunguzi kwa nguvu ya sumaku, na kupata taarifa za mwili mzima ndani ya dakika moja na kutoa majibu.

Na si jambo la ajabu kwa mgonjwa, baada ya kuona maajabu ya kifaa hicho, kushawishika kulipia fedha nyingi kadri atakavyotakiwa kwa ajili ya kugharimia tiba yake hata bila ya kudadisi ufanisi wa kifaa hicho na uwezo wake wa kutoa taarifa sahihi. Wananchi sasa hawaendi tena Loliondo kunywa kikombe cha babu, bali kwenye kliniki za tiba mbadala zinazotumia kifaa hicho kufanya uchunguzi.

Na kutokana na ukubwa wa matatizo ya hedhi na ugumba kwa wanawake na kuishiwa nguvu za kiume kwa wanaume, waganga hao wamekuwa wakieleza jinsi dawa zao zinavyoweza kumaliza matatizo yao kwa kutumia tiba mbadala na kupata wateja kila kukicha.

Na kwa kuwa wengi sasa wanamiminika kwenye kliniki hizo na kulipia kuanzia Sh320,000 kwa tiba ndogo hadi Sh700,000 kwa mkupuo, waganga wa tiba mbadala sasa wamekuwa na utajiri wa ajabu, mwandishi wa gazeti la The Citizen anaandika.

Mashine hiyo, ambayo inatengenezwa China na Korea Kusini, imekuwa ikitumiwa na waganga hao ili kubaini ugonjwa kabla ya kumuandikia dawa za asili ambazo watatakiwa watumie kutibu tatizo lao.

Kwa dakika chache ambazo mgonjwa atakuwa ameshikilia kidude mfano wa mpini wa kisu kilicho na waya uliounganishwa kwenye mashine hiyo sambamba na kompyuta, watengenezaji wanasema muda huo hutosha kukiwezesha kifaa hicho kukusanya taarifa nyingi za mwili na kutoa matokeo ambayo hutumiwa na waganga hao kutoa tiba.

Hata hivyo, licha ya matumizi yake yenye ukakasi wa kuaminika kwa matokeo ya uchunguzi wake, bado hakuna ushahidi wa kitaalamu uliothibitisha ufanisi wa mashine hiyo.

Kutokana na hilo na hatua ya Serikali kuvalia njuga suala la waganga hao na tiba wanazotoa, mwandishi wa The Citizen, ambalo ni gazeti dada la Mwananchi, alihudhuria kliniki zinatozotoa huduma hizo ili kuchunguza tiba hiyo na jinsi Quatum Magnetic Analyser inavyofanya kazi.

Katika uchunguzi wake mwandishi huyo alithibitisha matumizi ya mashine hiyo ambayo pia matumizi yake yalishatiliwa shaka na Baraza la Utoaji wa Tiba Mbadala la Tanzania (AHPCT) na kuagiza uchunguzi wa haraka ufanywe.

Mwandishi huyo alibaini kuwa mashine hiyo imekuwa ikutumiwa na madaktari hao kama kivutio cha soko lao kwa kuwaaminisha wagonjwa kuwa ina uwezo wa kuchunguza mwili mzima wa binadamu bila ya kumtoboa au kuchukua sampuli za damu au mkojo na kubaini sehemu yenye tatizo.

Mmoja wa wakazi wa jijini aliyewahi kwenda kwenye moja ya kliniki hizo, Jerome Sungura alisema alimpeleka mchumba wake baada ya kusumbuliwa kwa muda na maumivu makali ya tumbo.

Sungura, ambaye ni mkazi wa Mwenge, aliiambia The Citizen kuwa daktari aliyekuwapo siku hiyo aliwaambia ni lazima mchumba wake achunguzwe kwa kutumia mashine hiyo.

Kwa kuwa jina la mashine hiyo lilikuwa geni kwake, Sungura alimhoji jinsi mashine itakavyotumika kumchunguza mchumba wake.

Daktari alimuambia ingesaidia kuchunguza mwili mzima na kubaini tatizo liliko, kama ni kwenye ini, ubongo au mfumo wake wa uzazi.

Mganga huyo alimuambiwa Sungura kwamba mashine hiyo inatumika kwa siri kwa sababu haikuwa na kibali cha kutumika, hivyo Serikali ikifahamu itakuwa shida.

Baada ya maelezo hayo, Sungura aliridhia mchumba wake kupimwa na majibu kutoka baada ya dakika moja, yakieleza alibainika kuwa na ukosefu wa vitamin E na kutokuwa na usawa wa homoni mwilini (hormonal imbalance).

Hapo ndipo wawili hao walipotilia shaka mashine hiyo.

Hali kama hiyo ilimkuta Allan Semzaba ambaye gazeti la The Citizen lilimchukua ajifanye mgonjwa kwenye kliniki hiyo ikiwa ni sehemu ya uchunguzi huu.

Semzaba, ambaye ni baba wa watoto wawili, alifika kwenye kliniki hiyo na kumueleza mganga kuwa yeye ni tasa.

Semzaba alitakiwa kutoa Sh40,000 kwa ajili ya kugharimia kipimo na ada ya kuonana na daktari.

Baada ya vipimo daktari huyo aliyejitambulisha kwa jina moja la David, alimuambia Semzaba kuwa majibu yanaonyesha kuwa hana uwezo wa kupata mtoto.

Hivyo,i alimshauri atumie dawa za asili zenye thamani ya Sh 320,000 ambazo angempa akatumie kwa miezi mitatu na baada ya hapo tatizo la utasa lingeisha.

Hapo ndipo gazeti hili lilibaini kuwa mashine hizo hutumika kujipatia fedha si kusaidia wagonjwa.

Mapema mwaka huu Serikali mjini Dodoma iliwashikilia raia wawili wa Korea na kuwatoza faini ya Sh 500,000 kwa kutaka kutoa rushwa ili kliniki yao iliyokuwa inatoa huduma chini ya viwango isifungwe.

Licha ya juhudi za raia hao kugonga mwamba, Mwenyekiti wa AHPCT, Dk Edmund Kayombo alisema kushamiri kwa biashara hizo kunatokana na kutawala kwa vitendo vya rushwa katika uendeshaji wa kliniki hizo. Dk Kayombo alisema jambo hilo limekuwa kikwanzo kwa mamlaka husika kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahusika ambao ni wamiliki wa kliniki mashuhuri nchini.

“Tunafahamu kwamba baadhi ya wamiliki wa kliniki hizo wamekuwa wakiingiza na kutumia mashine ambazo tumekuwa tukizitilia shaka,” alisema Dk Kayombo kwenye mahojiano na The Citizen.

Pia alisema anafahamu kwamba matumizi ya mashine hizo yamekuwa yakiendelea kwa muda sasa.

“Tutafuatilia kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ili wachunguze kama mashine hizo zimesajiliwa na uhalali wa matumizi yake kwa sababu sisi tulifanya uchunguzi wetu tukabaini kwamba mashine hizo hazina msaada wowote kwa mgonjwa,” alisema Dk Kayombo.

Akizungumzia kuhusu tiba hizo, mtaalamu wa tiba asilia kutoka Hopitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Rogassian Mahunnah alitoa mfano wa tiba kwa mtu ambaye ni tasa akisema si rahisi kwa daktari wa tiba hizo kutibu ugonjwa huo kwa kutumia dawa hizo.

Alisema jambo hilo ni pana na kwamba dawa za asili zimethibitika kutibu magonjwa kama malaria na maumivu ya kawaida ya tumbo.

Post a Comment

(function(i,s,o,g,r,a,m){i['GoogleAnalyticsObject']=r;i[r]=i[r]||function(){ (i[r].q=i[r].q||[]).push(arguments)},i[r].l=1*new Date();a=s.createElement(o), m=s.getElementsByTagName(o)[0];a.async=1;a.src=g;m.parentNode.insertBefore(a,m) })(window,document,'script','https://www.google-analytics.com/analytics.js','ga'); ga('create', 'UA-87191200-1', 'auto'); ga('send', 'pageview'); ga('set', 'userId', {{USER_ID}}); // Set the user ID using signed-in user_id.
 
Top