0

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dr Hamis Kigwangalla, ameipongeza  Halmashauri ya Wilaya ya Njombe kwa kuboresha huduma katika kituo cha afya Lupembe baada ya  kukarabati chumba cha upasuaji na jengo la mama na mtoto.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe   ambapo alikagua kituo cha Afya Lupembe na Kichiwa ambapo katika kituo cha Afya Lupembe huduma ya upasuaji inatarajiwa kuanza muda wowote.

Akizungumza na wananchi katika Kata ya Lupembe na Kichiwa  mara baada ya kuweka jiwe la Msingi katika jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Lupembe, Dr .Kigwangalla alisema kuwa  ameridhishwa na namna  Halmashauri inavyotekeleza maagizo ya Serikali ikiwemo agizo la kila kituo cha Afya kuanzisha huduma za upasuaji agizo lililotolewa wilayani Meatu.

"Mimi ni mgumu sana kutoa pongezi na kwenye ziara zangu huwa sicheki, siwezi kucheka wakati wakinamama na watoto wanakufa, lakini panapofanyika mambo mazuri lazima tupongeze, hongereni sana kwa kuboresha huduma katika kituo cha afya Lupembe hasa chumba cha upasuaji, hongereni sana ." alisema Dr Kigwagala.

"Huduma zinazotolewa hapa  ni za kiwango cha hospitali ya Wilaya au Mkoa msione majengo yaliyo mkadharau ,kitaalamu tunaangalia huduma zinazotolewa . 

Uboreshaji huu utasaidia  kupunguza vifo vya akinamama na watoto kutokana na  kupunguza umbali wa kupata huduma za upasuaji maana nasikia zamani mlikuwa mnakwenda Hospitali ya Mkoa Kibena ambapo ni zaidi ya kilometa 60, sasa huduma zitapatikana hapa hapa" aliongeza Dr Kigwagala.

Dr kigwangalla alieleza kuwa serikali imeongeza mgao wa dawa na kuitaka  Halmashauri kuhakikisha inasimamia vizuri dawa zote zinazoletwa na kuwachukulia hatua wale wenye kukiuka maagizo ya Serikali.
Akijibu ombi la wananchi wa Kichiwa la kupatiwa gari la wagonjwa kwa ajili ya kituo cha afya, Dr kigwagala alisema kuwa suala hilo atalifanyia  kazi na pindi fursa itakapopatikana Halmashauri ya wilaya ya Njombe itapewa kipaumbele.

Kwa upande wake  Mbunge wa Jimbo la Lupembe lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe Bw. Joram Isamil Hongoli aliiomba Serikali kupitia  Naibu Waziri, Dr Kigwangalla kusaidia upatikanaji wa mashine za X-ray , Utra Sound pamoja na vifaa vingine muhimu katika vituo vya afya vya Halmashauri ya wilaya ya Njombe.

Halmashauri ya Wilaya ya Njombe  imeendelea kutekeleza sera ya kuwa na kituo cha afya katika kila  Kata  na  zahanati katika kila kijiji kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi pamoja na kuwahamasisha wananchi kuanza ujenzi wa vituo vya huduma  katika maeneo ambayo hayana.

Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imetenga shilingi 276,420,522 kupitia vyanzo vya mapato ya ndani na ruzuku kutoka serikali kuu kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati na kuanza ujenzi wa majengo ya upasuaji katika vituo vya afya vya Mtwango na Kichiwa ambapo vimetengewa  shilingi milioni 70  pamoja na kuanza kwa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.

Post a Comment

(function(i,s,o,g,r,a,m){i['GoogleAnalyticsObject']=r;i[r]=i[r]||function(){ (i[r].q=i[r].q||[]).push(arguments)},i[r].l=1*new Date();a=s.createElement(o), m=s.getElementsByTagName(o)[0];a.async=1;a.src=g;m.parentNode.insertBefore(a,m) })(window,document,'script','https://www.google-analytics.com/analytics.js','ga'); ga('create', 'UA-87191200-1', 'auto'); ga('send', 'pageview'); ga('set', 'userId', {{USER_ID}}); // Set the user ID using signed-in user_id.
 
Top